Maafisa nchini Iran waondoa uwezekano wa kufuta matokeo.
Radio Free Africa, all rights reserved 1995 - 2009
Chombo  kikuu   kinachoangalia  uchaguzi  nchini Iran  kimeondoa  uwezekano   wa  kufuta  matokeo ya  uchaguzi  wa  rais  wakati  dunia  inaeleza wasi wasi  wake katika  ukandamizaji  wa  nguvu  wa maandamano  ya   wapinzani  wanaotoa changamoto  kubwa  kwa  utawala    wa   Kiislamu nchini  humo  uliodumu  sasa  kwa  muda  wa  miaka 30.

Msemaji  wa  baraza  la   wadhamini   Abbasali Kadkhodai  amenukuliwa  akisema  kuwa  katika uchaguzi  wa  hivi  karibuni  wa  rais  tumeona hakuna  udanganyifu  ama  ukiukaji  wowote.

Upande  wa  upinzani  umekuwa  ukifanya maandamano   karibu  kila  siku, wakidai  kufanyika udanganyifu  na  mapungufu  kadha   katika uchaguzi  wa  hapo  Juni  12  ambao  umemrejesha rais  mwenye  msimamo  mkali  Mahmoud Ahmadinejad  madarakani  kwa  muda  wa  miaka minne  mingine.

Viongozi  wa  dunia  wanatoa   miito  ya  kusitishwa mara  moja  kwa   matumizi  ya  nguvu yanayofanywa  na  serikali  dhidi  ya  waandamanaji, huku  vyombo  vya  habari  vya   taifa  vikiripoti  kuwa kiasi  watu  17  wameuwawa   na  wengine  wengi wamejeruhiwa  katika  ghasia  hizo  ambazo zimelikumba  taifa   hilo  kwa  muda  wa  siku  11 sasa.

Mitaa  ya  mjini  Tehran  imeendelea  kuwa  na  hali tete  leo  Jumanne  siku  ambayo  maelfu  ya   polisi wa  kuzuwia  ghasia   wakiwa  na  virungu  vya chuma  na  wakifyatua  mabomu  ya  kutoa  machozi, wengi  wakiwa  katika  pikipiki, walivunja maandamano  ya  wapinzani  wapatao  1,000. Msemaji  wa   Ikulu  ya  Marekani  Robert  Gibbs akiulizwa  kuhusu  rais   hisia  za  rais  Barack Obama  kuhusu  maandamano  hayo  alisema.

Ametiwa  moyo  na  kile  tulichokiona  katika televisheni. Nadhani  hasa  ni  kuhusu  picha zinazoonyesha  wanawake  nchini  Iran  ambao wamejitokeza  kutekeleza  haki  yao  ya kuandamana, kutoa  mawazo  yao  na  kusikika.

Katibu  mkuu  wa  umoja  wa  mataifa  Ban  Ki-moon ameeleza  wasi  wasi  wake  mkubwa  juu  ya  ghasia hizo  na  kutoa  wito  wa  kusitishwa  mara  moja  kwa hatua  za  kuwakamata  waandamanaji, vitisho  na matumizi  ya  nguvu. Ameitaka  serikali  na wapinzani  kutatua   matatizo  yao  kwa  njia  ya amani  na  mazungumzo  pamoja  na  njia  za kisheria.

Baadhi  ya  nchi  za  Ulaya  zimeanza  kuwataka  raia wao  kujiepusha  kwenda  Iran,  nchi  ambayo imekumbwa  hivi  sasa  na  mzozo  mkubwa  tangu mapinduzi  ya  Kiislamu  miaka  30  iliyopita  mzozo ambao  unatishia  msingi  wa  taifa  hilo  la  Kiislamu.

Wakati  huo  huo   chama  cha  wanafunzi  wa  Iran kimefuta  maandamano  yaliyopangwa  kufanyika  nje ya  ubalozi  wa  Uingereza  mjini  Tehran  leo Jumanne  baada   ya  kupigwa  marufuku  na maafisa  wa  nchi  hiyo.

Nae  kiongozi  wa  upinzani  nchini  Iran  Mir Houssein  Mousavi  amekutana  na  viongozi  wa  juu wa  kidini  na  kujadiliana  nao  kuhusu  hali  ya mambo  nchini  humo, ikiwa  ni  pamoja  na  vifo  vya waandamanaji  wakati  wa  maandamano  mitaani mjini  Tehran.

Katika  mkutano  huo  uliofanyika  jana  Mousavi amejadili  kuhusu  uchaguzi  wa  Juni  12, haki  za raia  kufuatilia  suala  hilo, ukamataji  wa  watu holela  na  mashambulizi  dhidi  ya  waandamanaji ambayo  yamesababisha  vifo  vya   watu  wasio  na hatia.

Wakati  huo  huo  duru  katika  wizara  ya  mambo ya  kigeni  nchini  Iran  zimekanusha  kuwa  balozi wa  Uingereza  nchini  humo  amerejeshwa  nchini mwake  kwa  mashauriano.

Rais  pamoja  na  baraza  lake  la  mawaziri wataapishwa  mbele  ya  jengo  la  bunge  kati  ya tarehe  26  Julai  na  August  19  kufuatia  uchaguzi wa  rais, limesema  shirika  la  habari  la  Iran  IRNA leo  Jumanne
































.







.







.





.