WATU wanne wamekufa papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka katika shughuli za mazishi kuacha njia na kugonga mti kisha kupinduka huko Mbwewe wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 11 jioni ya kuamkia leo Agosti 12 katika barabara kuu ya Segera- Chalinze wilayani humo.
Ajali hiyo imehusisha gari namba T 906 BET Toyota Coaster iliyokuwa ikiendeshwa na Idrisa Mtoro (33) mkazi wa Tanita Kibaha na kwamba alikuwa akitokea Moshi kwenda jijini Dar esalaam kwa shughuli za mazishi.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Absaloom Mwakyoma amedhibitisha ajali hiyo ambapo aliwataja abiria waliokufa katika ni Hussein Idd(20) fundi umeme na mkazi wa Lushoto Tanga,Bakari Wilson maarufu kwa jina Kitonga(24) mkazi wa Mwanga Kilimanjaro,Ismail Kadiria(18) mkazi wa Kisaru Kilimanjaro.
Mwingine aliyefariki katika ajali hiyo ni mwanamke mtu mzima anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30 -35 na hajafahamika jina lake na kwamba miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali teule ya Tumbi Kibaha kusubiri ndugu.
Kamanda Mwakyoma pia amewataja majeruhi hao wawili kuwa ni Zaina Musa mkazi wa Makuyuni Tanga na Lena Kadiria (20) mkazi wa Mika Moshi na wote wamelazwa Tumbi kwa matibabu zaidi na hali zao hadi mchana leo zilikuwa zinaendelea vema.
Mwakyoma amesema chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa na kwamba dereva Idrisa alikimbia mara baada ya tukio hilo na alijisalimisha jana asubuhi Polisi hivyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.
Radio Free Africa, all rights reserved 1995 - 2009