Uchunguzi uliofanywa na Radio Free Africa umebaini kuwa wagonjwa wengi ni wakazi wa vijiji vya Songambele, Ronsoti, Sabasaba, Nyamisangura, Rebu na Tagota.
Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Dk. Winani, Tatu Manyama, amesema zaidi ya wagonjwa 50 wa kipindupindu wameshalazwa hospitalini hapo tangu ugonjwa huo ulipuke wiki iliyopita.
Dk. Charles amesema idadi ya wagonjwa wa kipindupindu imekuwa ikiongezeka na kupungua katika Hospitali ya Wilaya na kwamba zaidi ya wagonjwa 40 wameshatibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Katika juhudi za kukabili ugonjwa huo, Dk. Charles amesema wataalamu wa afya wameshaweka dawa ya kutibu maji kwenye visima 100, wamefunga migahawa 17 ya kuuza chakula na zaidi ya vilabu 10 vinavyouza pombe za kienyeji mjini Tarime.
Wataalamu wa afya pia wanaendelea kuelimisha wananchi jinsi ya kujikinga na kipindupindu ikiwa ni pamoja na kuwahimiza kuchemsha maji ya kunywa, kunawa maji ya moto kabla ya kula na baada kutoka chooni.
Chanzo cha mlipuko wa ugonjwa huo, kwa mujibu wa Dk. Charles, ni matumizi ya maji machafu ya visima katika kipindi hiki cha kiangazi.
Radio Free Africa, all rights reserved 1995 - 2009