UPIGAJI wa kura za kumkataa ama kutomkataa mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Bunda, Pastory Ncheye, leo jumatatu umeahirishwa tena, baada ya kutaka kutokea uvunjifu wa amani kutokana na kambi mbili kupingana vikali.
Upigaji kura huo ulikuwa ufanyikie leo kwenye ukumbi wa Annex Manjebe, ulioko mjini Bunda, kwa kushirikisha wananchi zaidi ya 1, 800 wa kitongoji cha Kabarimu, ambapo lengo la upigaji kura hizo ni kutaka kuona ni wananchi wangapi ambao hawamtaki mwenyekiti huyo, ambaye pia ni mwenyekiti wa kitongoji hicho.
Ilikuwa ni majira ya saa 4:00 asubuhi wananchi walikuwa tayari wamekwishaingia katika ukumbi huo, huku baadhi ya watu wengine ambao wanadaiwa kuwa si wakazi wa kitongoji hicho, wakidaiwa kujipenyeza ili pia waweze kupiga kura.
Kufuatia hali hiyo viongozi wa wilaya, akiwemo afisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Bunda, Willam Mabaga na msimamizi wa uchaguzi huo, afisa tarafa ya Sereneti, Justine Rukaka, walitoa tangazo la wananchi wanaostahili kupiga kura, kwamba ni wakazi wa kitongoji hicho tu na si vinginevyo.
Ghafula hali ilibadilika na ndipo watu waliokuwa nje ya ukumbi huo na baadhi ya waliokuwa ukumbini humo, walianza vurugu za kuzomea zomea na kuizonga meza kuu, hali iliyaashilia kuvunjika kwa amani.
Kutokana na vurugu hizo msimamizi wa zoezi hilo Justine Rukaka, alijaribu kuwatuliza na kuwapa utaratibu unaotakiwa, lakini upande wa pili unaodaiwa kwamba sio wakazi wa kitongoji hicho na wanaodaiwa kumuunga mkono mwenyekiti huyo, walizidisha vurugu ya kuzomea zomea.
Inadaiwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wamenunuliwa kwa kitu kidogo na baadhi yao kunywesha pombe, kwa lengp la kuvuruga zoezi hilo, ili lisifanyike.
'Kuna baadhi ya watu tumesikia wamenunuliwa na baadhi yao tayari wamekunywa pombe, ili kutuvuruga, sasa mimi ninasema waendelee na tunawaona' ilisikika sauti ya Rukaka.
Ni kufuatia dalili zote za kuwepo uvunjifu wa amani, msimamizi wa zoezi hilo, Rukaka alitangaza kuhairisha zoezi hilo mpaka itakapotangazwa tena baadaye.
'Tumewaelekeza jinsi ya utaratibu unaotakiwa, lakini naona baadhi ya watu hawanielewi, sasa nafikiri kuna kitu kingine hapa maana hata wengine si wakazi wa kitongoji Kabarimu....mfano mke wa mwalimu wewe. Sasa natangaza rasmi kuhairisha zoezi hili mpaka hapo baadaye' alisema Rukaka.
Baada ya zoezi hilo kuhairisha wananchi wanaodaiwa kuwa si wakazi wa kitongoji hicho, walimbeba juu juu, Ncheye huku wakishangilia.
Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Kabarimu, waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, walisikika wakisema kuwa hata kama wakimshabikia kutaka kuwapotosha, lakini bado msimamo wao ni ule ule wa kumkataa mwenyekiti huyo.
'Hawa wanajisumbua tu, sisi ndio wakazi wa kitongoji hiki hata kama wakimshabikia ni kazi bure tu, msimamo wetu ni uleule wa kumkataa, ili wengine wakichaguliwa wasiwe na tabia kama yake' alisema mwananchi mmoja.
Juhudi za kuzungumza na Ncheye, katika eneo hilo ili atowe msimamo wake kuhusu sakata hilo, hazikuzaa matunda kutokana na watu wa kundi lake kumuinua juujuu na kuanza kukimbia naye kuelekea nyumbani kwake.
Aidha, alipopigiwa simu ili azungumzie suala hilo, simu yake ya mkononi iliita mpaka ikakatika, na alipopigiwa kwa mara ya pili, alijibu kwa mkato kwamba 'wewe peleka jinsi unavyojua mbona ulikuwa unapeleka peleka tu' na akakata simu.
Hivi karibuni wakazi wa vitongoji vitatu vya Kabarimu, Majengo na Chiringe, walitangaza azma yao ya kumkataa mwenyekiti huyo, kwa madai kuwa hashiriki kwenye kusaka wahalifu, pindi yowe inapopigwa na pia baadhi ya wananchi aliwanyima mahindi ya msaada, licha ya kuwachangisha sh. 600, kwa kila mwananchi.
Ni kufuatia hali hiyo mkuu wa wilaya ya Bunda, Francis Isack, aliwaambia wananchi hao kuwa jukumu la kumkataa mwenyekiti huyo liko mikononi mwa wananchi wa kitongoji cha Kabarimu na akawataka wapige kura ili kujua ni wanagapi ambao hawamtaki, ili hatua zichukuliwe.
.