Mamlaka ya Mapato nchini TRA mkoani Mbeya imesema kuna changamoto kubwa ya kukomesha biashara za magendo zinazofanyaka katika mpaka wa Tanzania na Zambia wa Tunduma upande wa Tanzania na Nakonde nchini Zambia.
Kaimu Meneja wa TRA mkoani Mbeya Bw. Brayton Mkamba amesema kuwa shilingi bilioni 19.5 zinazotokana na ushuru wa forodha hukusanywa mpakani hapo kwa mwaka kiasi ambacho ni kikubwa kuliko mapato yanayokusanywa katika mipaka mingine hapa nchini.
Bw. Mkamba amesema hayo mpakani Tunduma wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amekiri kuwepo changamoto kubwa ya upotevu wa mapato kutokana na bidhaa nyingi kuvushwa kwa njia za magendo mpakani hapo.
Amesema kutokana na mpaka huo kuwa na njia nyingi zisizo rasmi ambazo hutambulika kama ‘njia za panya’ baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wametumia mwanya huo kuvusha bidhaa bila kulipia ushuru wa forodha hali mabayo amesema inawapa wakati mgumu maofisa wa TRA na forodha kudhibiti hali hiyo.
Hata hivyo kaimu meneja huyo wa TRA mkoani Mbeya, amesema hatua zinazochukuliwa na serikali mbili za Tanzania na Zambia kujenga kituo cha biashara kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara mpakani hapo itakuwa ni hatua ya muhimu katika kudhibiti magendo katika mpaka huo.
Akizungumzia kikithiri kwa biashara za magendo mapakani Tunduma Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya viwanda, biashara na masoko Dakt. Shaaban Mwinjaka amesema serikali zote mbili zimedhamiria kukomesha magendo katika mpaka huo kwa kushirikiana katika kushughulikia uondoshaji mizigo ili kupunguza msongamano.
.
Radio Free Africa, all rights reserved 1995 - 2009
Na Fredy Bakalemwa , Tunduma Mbozi Mbeya