IGP Mwema aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Tatwe, wilayani Rorya na Kitenga wilayani Tarime ambavyo vimekumbwa na mapigano yaliyosababisha vifo vya watu 31 wakiwamo akinamama na watoto. Alisema kushamiri kwa vitendo vya wizi wa mifugo mkoani Mara, ni tatizo ambalo litashughulikiwa kwa nguvu zote za kidola.
Alisema kama lilivyoshughulikiwa tatizo la uvamizi na wizi kwenye benki nchini, Jeshi la Polisi pia litalichukulia tatizo la wizi wa mifugo mkoani hapa kama walivyofanya katika kukomesha wizi wa benki.
Alisema wananchi wa maeneo ya wilaya za Tarime na Rorya, wanaifanya mifugo kama hifadhi ya fedha zao, kwa maana ni sehemu ya benki zao na hivyo suala la wezi kuipora ni hatua ambayo inachukuliwa kama tatizo lingine la kijinai.
“Mapigano na mauaji yanayotokea mara kwa mara mkoani hapa yanachochewa na wizi wa mifugo, hivyo Polisi tutafanya kila liwezekanalo kukomesha vitendo hivyo,” alisema IGP Mwema. Alisema ataishawishi serikali kuongeza vitendea kazi hasa magari na redio za mawasiliano kwa askari ili kurahisisha ufuatiliaji wa matukio hayo.
Awali, Mbunge wa Rorya, Profesa Philemon Sarungi, alimwambia Mkuu wa Jeshi la Polisi kuwa Wajaluo hawana ugomvi na Wakurya bali wananchi wa jamii ya Kijaluo wanapambana na wezi wa mifugo.
Hata hivyo, Profesa Sarungi alimuomba IGP Mwema kuangalia uwezekano wa kuongeza vituo vya Polisi katika maeneo mbalimbali wilayani Rorya na Tarime ili kudhibiti wizi wa mifugo katika wilaya hizo.
Hoja za ujenzi wa vituo vya Polisi pia zilitolewa na wananchi wa Kijiji cha Kitenga wilayani Tarime kama hatua za kutaka kukomesha uhalifu, ukiwemo wizi na mauaji kwa watu wasio na hatia.
Wakizungumza kwenye mkutano wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, wakazi wa kijiji hicho wameliomba Jeshi la Polisi kuangalia uwezekano wa kuweka vituo vya Polisi katika maeneo tete ili kukomesha wizi wa mifugo na mapigano ya mipaka.
Kabla ya mikutano hiyo, IGP Mwema akitumia helikopta ya Jeshi la Polisi alikagua maeneo mbalimbali ya mapigano na kujionea mwenyewe nyumba zilizoteketezwa kwa moto katika vijiji mbalimbali.
Katika ziara hiyo, IGP alifuatana na Mkurugenzi wa Operesheni, Kamishna Paul Chagonja, Mkuu wa Operesheni Maalumu, Naibu Kamishna Venance Tossi na Mkuu wa Sera na Maendeleo ya Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi Mwandamizi Paul Ntobi na Mkuu wa Majanga wa Jeshi hilo, Mrakibu Mwandamizi Nasser Mwakamboja.
.
.
.