Kutoka Bungeni Spika Sitta amtetea Mhe. Selelii
 
Radio Free Africa, all rights reserved 1995 - 2007
Alisema hayo jana, wakati akitoa mwongozo wake baada ya kuombwa kufanya hivyo na Selelii ambaye Juni 15 mwaka huu, alihoji uhalali wa fedha hizo kutumika kwenye mradi wa ujenzi wa barabara hizo kabla ya kuidhinishwa na Bunge.

Spika Sitta ambaye alitoa mwongozo huo kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali na majibu jana, alisema kuwa fedha zinazotumika kwenye mradi wa ujenzi huo, hazitokani na fedha zinazoombwa mwaka huu wa fedha wa 2009/2010 bali ni fedha zilizoidhinishwa na Bunge mwaka wa fedha wa 2008/2009.

“Hata hivyo, hoja ya Lucas Selelii ina msingi, kwa sababu alipopitia kitabu cha miradi ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha 2009/2010, ukurasa wa 189, item 4189, inaonyesha kuwa kwa miaka ya nyuma, hakuna fedha zilizotengwa, jambo lililomfanya aamini kuwa matengenezo yanayoendelea hivi sasa yanatokana na fedha zinazoombwa kwa mwaka huu wa fedha na ambazo hazijaidhinishwa na Bunge hili,” alisema Spika Sitta.

Akifafanua suala hilo, Sitta alisema mchakato wa kutengeneza barabara hiyo, ulianza mwaka 2006 na fedha zake jumla ya sh bilioni 10.4 ziliidhinishwa na Bunge mwaka 2006/2007, kwa matarajio ya kukamilisha usanifu na kuanza ukarabati wa barabara hiyo.

Alisema kazi ya ukarabati inayoendelea sasa, fedha zake ziliidhinishwa na Bunge katika mkutano wa 12 na fedha zilizoombwa katika mwaka ujao wa fedha 2009/2010 sh 22,844,500,000 ni kwa ajili ya kufanyia ukarabati mkubwa wa barabara hii kwa fedha za DANIDA ambazo ni sh bilioni 17.6 na sh milioni 50 fedha za ndani.

“Lakini ukitazama ukurasa husika wa 189, alioutaja Selelii, mradi wa ukarabati wa barabara ya Chalinze- Segera-Tanga kwa mwaka wa fedha 2007/2008 na 2008/2009, hakuna fedha zilizotengwa ila mwaka huu wa fedha 2009/2010, inaonyesha kiasi cha fedha kilichotengwa ni sh 22,844,500,000.

“…Hivyo Selelii alikuwa na haki ya kutaka ufafanuzi wa matumizi ya fedha za mradi kama ilivyokuwa inaripotiwa katika vyombo vya habari.

“Kwa kuwa utata huo unatokana na mabadiliko ya miundo, ni ushauri wangu kuwa ili kuondokana na matatizo kama haya kunapotokea na mabadiliko ya miundo ndani ya wizara, hasa mabadiliko yale yanayohusiana na miradi mikubwa, ni vema fedha zinazotengwa katika miradi ya aina hiyo, zikabainishwa kwa uwazi zaidi katika vitabu vya bajeti,” alisema Spika Sitta.

Endapo Selelii angethibitika kusema uongo, alikuwa akikabiliwa na adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria mkutano mmoja wa Bunge, kama ilivyotokea mwaka 2007 kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliyesimamishwa kuhudhuria mkutano mmoja wa Bunge baada ya Bunge kubaini kuwa alisema uongo kuhusu kusainiwa kwa mkataba wa mgodi wa madini wa Buzwagi nje ya nchi katika mazingira ya rushwa.





















     

.
.



.