Myanmar yatoa msamaha kwa wafungwa.
Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya wanawake na maendeleo (WAMA) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari 22 mkoani Tabora, ili kuweza kusaidia jamii ipunguze kiwango cha maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Akizungumza katika mafunzo hayo ya siku moja Afisa wa WAMA Neema Mhada, alisema kuwa shirika hilo liko tayari kufanyakazi kwa ukaribu na waandishi wa habari kwa sababu linaamini kwamba waandishi wa habari ni watu muhimu katika kufikisha ujumbe kwa jamii.

Neema, alisema kuwa kinachotokea katika maambukizi hayo ni kwamba wanawake wengi wanaoishi na virusi vya ukimwi, wengi wao wamekuwa hawajui jinsi wanavyowaambukiza watoto wao jambo ambalo alisema linahitaji kutangazwa zaidi na zaidi ili liweze kufahamika.

Alisema wanawake wanapaswa kutambua kuwa maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yanafanyika katika hatua kuu tatu ambazo ni wakati mtoto akiwa tumboni, wakati wa kuzaliwa na wakati wa kunyonyeshwa.

Alisema hata hivyo kulingana na maaendeleo ya kisayansi hivi sasa, maambukizi hayo yote yanaweza kuepukwa na kuwafanya watoto wanaozaliwa na akinamama hao kutokuwa na virusi vya ukimwi na hivyo kuishi maisha mazuri zaidi.

Alisema wanawake wanaweza kuepukana na kuambukiza watoto wao iwapo kama watapatiwa elimu kuhusu maambukizi hayo na kupatiwa dawa zinazozuia maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika hatua kuu mbili ambazo ni mtoto akiwa tumboni na wakati wa kujifungua.

Alisema pia mtoto aliyezaliwa salama anaweza kutoambukizwa ukimwi iwapo kama hata nyonyeshwa na mama yake mwenye virusi vya ukimwi, hivyo kusababisha mtoto huyo atapatiwe vyakula vyenye viinilishe hitajika katika mwili wa mtoto.

Alisema elimu hii inapaswa kusambazwa kote nchini sanjari na kitendo cha kupima virusi vya ukimwi kwa hiari ili kuweza kuwatambua watu walioathirika na ukimwi na kuwasaidia wasiweze kuambukiza wengine na kutumia dawa katika muda muafaka.

Hata hivyo Neema, aliitaja changamoto kubwa inayowakabili WAMA hivi sasa ni wanaume wengi kutokubali kupima afya zao kitu ambacho alisema kinasababisha maambukizi ya ukimwi yasiweze kudhibitiwa kwa urahisi.
Radio Free Africa, all rights reserved 1995 - 2009